Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Hebron
Mwakagenda amesema wameazimia kufungua kesi ya kudai haki ya kufanya maandamano
ya amani nchini baada ya maandamano yao yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Oktoba
30, mwaka huu kuzuiliwa na Jeshi la Polisi.
Mwakagenda amesema Oktoba 7, mwaka huu walitoa tamko kwa
umma la kukusudia kufanya maandamano ya amani nchi nzima kumpongeza na kuunga
mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusimamia rasilimali za taifa
pamoja na kupiga vita rushwa lakini Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam liliwazuia.
Pia maandamano hayo yalilenga kufikisha ujumbe kuhusu haja
ya serikali kurejesha mchakato wa katiba mpya ili taifa liweze kupata katiba
mpya chini ya uongozi wa Rais Magufuli lakini jitihada zao ziligonga mwamba.
“Kwa uzito huu JUKATA tulimwandikia Rais Magufuli ili
ayapokee maandamano hayo ambayo yalikuwa yamepangwa kuanzia ofisi zetu zilizopo
Mwenge hadi Viwanja vya Mnazi Mmoja, hadi leo hatujapata majibu ya barua
iliyotumwa Ikulu kwa Rais Magufuli juu ya ombi letu. Lakini tulipokea barua
kutoka Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ikikataza kufanyika kwa maandamano
hayo ya c amani,” amesema Mwakagenda.
Jeshi la Polisi lilizuia maandamano hayo kwa sababu tatu,
zikiwemo kwamba Rais Magufuli hakuthibitisha kushiriki kwenye maandamano hayo,
kufanya maandamano umbali mrefu kutoka Mwenge hadi Mnazi Mmoja kutaathiri
shughuli kwa kufunga barabara na Oktoba 30 ndiyo siku ambayo mitihani ya kidato
cha nne ingekuwa ikifanyika.
“Kwa sababu hizi zilizotumika kukataza maandamano, tumefikia
maamuzi ya kwenda kufungua kesi mahakamani kudai haki ambayo inaminywa na
kukandamizwa na Jeshi la Polisi kwa kutumia sababu nyepesi.
“Tupo kwenye hatua za mwisho kutekeleza uamuzi huu na kwamba
jopo la mawakili wasomi wasiopungua kumi wakiongozwa na Dkt. Rugemeleza Nshala
watahusika katika mchakato huu wa kudai mahakamani haki hii ya kufanya
maandamano ya amani,” alifafanua.
Mwakagenda alihitimisha kwa kusema Tanzania inafuata misingi
ya kidemokrasia na utawala wa sheria ambapo misingi mikuu ya kidemokrasia ni
pamoja na uhuru wa watu kukusanyika na kujadiliana kwa mujibu wa sheria
kujadili masuala yanayohusu taifa lao.
No comments:
Post a Comment