Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi TFDA imetakiwa
kuboresha udhibiti wa uingizaji wa Dawa, Vipodozi na Chakula nchini kiholela
ili kulinda afya ya Watannzania.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa kuzindua Cheti Cha Mfumo
wa Uhakiki Ubora wa Huduma katika kiwango cha kimataifa cha ISO 9001-2015 leo jijini Dar es Salaam.
“Dawa ni kitu nyeti sana, hatuwezi kuruhusu dawa feki
kuingia nchini, mnafanya kazi nzuri sana katika nyanja hii na muendelee na
mpango huu ili kudhibiti uingizaji wa vyakula visivyokidhi viwango na mahitaji
ya watanzania,” amesema Dkt. Ndugulile.
Aidha Ndugulile amesema kuwa TFDA wanatakiwa kuzingatia
muongozo wa kupitisha vyakula na vipodozi kwenye mipaka ya nchi kwa kuzingatia
ubora na viwango vilivyoweka katika kudhibiti uingizaji mbovu wa vyakula.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Bw. Hiiti Silo
amesema kuwa ili kuendelea kukidhi matakwa ya wateja na mahitaji yao wameamua
kuendana na kiwango cha kimataifa na kuwaita ISO kuja kuhakiki ambapo
wamefanikiwa kukidhi na kupata cheti.
“Shirika la Viwango la Kimataifa ISO limehakiki ubora wa
huduma zetu katika kukidhi mahitaji na matakwa ya watumiaji wa huduma zetu na
kutupatia cheti kinachoturuhusu kutoa huduma nchini,” alisema Bw. Silo.
Aidha Bw. Silo amesema kuwa wapo bega kwa bega na Serikali
ya awamu ya tano ianyoongozwa na Rais Dkt. John pombe Magufuli katika kusogeza
mbele gurudumu la afya hapa nchini kupitia taasisi ya TFDA.
No comments:
Post a Comment