Chama cha ACT Wazalendo kimeweka wazi msimamo wake kuhusu
suala la kujiunga na UKAWA ambapo kimesema suala hilo ni pana na lazima
lizingatie maslahi ya chama.
Katibu Kamati ya Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa chama
hicho Ado Shaibu, amesema suala la kujiunga au kutojiunga UKAWA litaamuliwa na
wanachama na viongozi.
“Ni kweli kila mtu anazungumza yake kuhusu msimamo wa chama
chetu lakini ukweli ni kwamba kwa hali ya kisiasa ilivyo nchini kuna mambo
yanalazimu vyama vya upinzani vishirikiane, lakini ikija suala la kujiunga
UKAWA lazima ujue maslahi ya chama ndani ya umoja huo”, amesema Ado Shaibu.
Ado ameongeza kuwa ikifikia wakati kuna ulazima wa ACT
Wazalendo kujiunga na UKAWA basi suala hilo litaamuliwa na viongozi pamoja na
wanachama.
Kwa upande mwingine Shaibu amewataka wanachama wa ACT
Wazalendo kuendelea kukiunga mkono chama hicho wakati huu ambao sera zake
zimejikita zaidi kwenye kuutafuta uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara kwani
ndio njia pekee ya kuongea na wananchi moja kwa moja.
No comments:
Post a Comment