Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waishio
Canada wadumishe mshikamano wao na wawe na uzalendo kwa Taifa lao.
Waziri Mkuu ambaye yuko Canada kwa ziara ya kikazi,
wakati akizungumza na watanzania waishio nchini humo amesema kila Mtanzania
anapaswa ahubiri utaifa wake.
“Tembea huku ukiringia nchi yako, wakati wote ringia nchi
yako, unapotakiwa kuisemea nchi yako, isemee vizuri kama ambavyo wengine
wanasemea vizuri nchi zao licha ya matatizo waliyonayo.”
Amewataka pia wakumbuke kuweka akiba na wanapopata fursa
watume fedha zao nyumbani ili zisaidie kuleta maendeleo.
“Ukipata kitu kidogo, rusha nyumbani; ukipata mtu anayeweza
kuleta tija, mlete nyumbani, nasi tutawapokea wewe na yeye,” alisisitiza.
“Tunawasisitiza muitangaze nchi yetu kwa mataifa mengine ili
nao waone Tanzania ni mahali pa fursa, na akitaka kuwekeza ajue kuwa anawekeza
mahali ambapo ni salama,” amesema.
Alisema Serikali inasisitiza wananchi waishio nje ya nchi,
wawe wazalendo na washirikiane kuhakikisha wanazitumia vizuri fursa za
kimaendeleo kwa manufaa ya nchi yao.
Awali, Balozi wa Tanzania nchini Canada, Jack Nzoka,
alitumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania waishio nchini humo wazingatie sheria
za nchi hiyo.
“Wote sisi tunawatambua kama mabalozi katika nafasi zenu
hapa Canada. Tunawashauri muwe raia wema, na muishi kwa kufuata sheria na
taratibu za nchi hii na msisahau mlipotoka, kwani hakuna mahali pazuri kama
nyumbani,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment