Serikali imewataka Wataalam wa
Maendeleo ya Jamii kurejesha ari na hamasa ya jamii kushiriki katika kazi za
maendeleo ili kutoa mchango katika kufikia Tanzania ya Viwanda na yenye uchumi
wa kati.
Kauli hii imetolewa MJini Dodoma na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa 12 wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii unafoanyika katika
ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.
Ummy Mwalimu amesema
kuwa kupitia Mkutano huo Wataalam wa Maendeleo ya Jamii
wanatakiwa kutoa mapendekezo kuhusu mbinu bora
zitakazosaidia kurudisha ari na hamasa ya jamii kushiriki katika maendeleo na
hivyo kusaidia kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Ummy Mwalimu amefafanua kuwa
wataalam wa maendeleo ya jamii ndiyo wenye jukumu la kuhamasisha utekelezaji wa
miradi ya kisekta hususan kilimo, afya, elimu, na miundo mbinu na kadhalika.
“Wataalam wa Maendeleo ya Jamii watumie fursa hii
kujitathmini ili kupata majibu ya namna bora ya kutekeleza majukumu yao ya
kuamsha ari ya wananchi kushiriki kwenye uzalishaji na kutokomeza ukatili wa
jinsia ambao unapunguza kasi ya kufikia uchumi wa kati na maendeleo jumuishi,”
amesema Ummy.
Naye Katibu Mkuu Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga amesema kuwa katika awamu ya
sasa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wana wajibu wa kuelimisha na kuamsha ari
ya wananchi kufanya kazi za uzalishaji kwa bidii kwa kuzalisha mali ghafi
zinazohitajika na viwanda na kuwekeza kwenye viwanda vidogo vidogo na vya kati.
Bibi Sihaba Nkinga amefafanua kuwa
malengo ya Mkutano huo umezingatia tathmini ya mchango wa Sekta ya
Maendeleo ya Jamii katika kuamsha ari na hamasa ya wananchi
kushiriki na kuchangia maendeleo kwa kushirikiana na viongozi wa Sekta na Idara
nyingine katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amewaasa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kwa
kushirikiana na wadau kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujitoa
katika kufanya kazi za kujiletea maendeleo katika maeneo yao.
Lengo la Mkutano huu wenye kauli mbiu isemayo “Amsha
Ari ya Ushiriki wa Wananchi Kufikia Uchumi wa Viwanda” ni
kuhakikisha Wizara na wadau wanashirikiana katika kuamsha ari ya wananchi
kufanya kazi za maendeleo na kusimamia Mpango ya kutokomeza ukatili wa jinsia
ambao kwa kikasi kikubwa unapunguza kasi ya Taifa kufikia uchumi wa
viwanda.
No comments:
Post a Comment