Klabu ya Mbeya City imesema kuwa haiwawaogopi wala hawatishwi
na washambuliaji wa Wekundu wa Msimbazi, Emmanuel Okwi na Laudit Mavugo.
Kocha wa Mbeya City, Ramadhan Nsanzurwimo amesema amejipanga
vizuri kuhakikisha wanashinda dhidi ya Simba bila ya kuwahofia nyota
wake Okwi raia wa Uganda na Mavugo raia wa Burundi.
“Maandalizi ya kucheza na Simba yanaendelea vizuri, Simba ni
timu kubwa lakini kwetu haitokuwa mechi nyepesi kwa sababu tumewaona
katika mchezo uliopita wakicheza na Yanga.
“Tunataka ushindi na hatuwezi kuhofia mchezaji wao mmoja
mmoja, hatuna cha kuogopa, wachezaji wao wote ni wa kawaida na wapo kwenye
kiwango kimoja,” amesema Nsanzurwimo.
Nsanzurwimo, raia wa Burundi, alijiunga na Mbeya City hivi
karibuni kuchukua nafasi ya Kinnah Phiri aliyetimuliwa lakini amefanikiwa
kukaa benchi kwenye mechi mbili.
Mechi ya Mbeya City na Simba ambayo ni namba 72 katika Ligi
Kuu Bara msimu huu, itachezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na
tayari Simba imeshaingia Mbeya tangu jana.
No comments:
Post a Comment