Ziara yake ya leo imelenga kubaini changamoto za kiforodha na kikodi zinazosababisha kuminywa kwa fursa za kiuchumi kati ya wananchi wa pande mbili za Muungano.
Baadhi ya changamoto kubwa kwa sasa ni utozwaji mara mbili wa kodi ya VAT kwa wafanyabiashara wanapoingiza na kutoa mizigo yao kati ya Tanzania bara na Visiwani. Pia changamoto za wananchi wa Zanzibar pale wanapotaka kuingiza na kutumia vyombo vyao vya usafiri upande wa Tanzania bara pamoja na viwango tofauti vya ukadiriaji wa kodi kwa wafanyabiashara wanapoingiza mizigo kutoka nje ya nchi kwa kutumia bandari ya Dar es salaam na bandari ya Zanzibar.
Waziri Makamba amesema kuwa moja ya shabaha za Muungano ni kufungua fursa za ustawi wa watu wa pande zote mbili na kwamba mifumo ya kodi haipaswi kuminya fursa hizo na kuahidi kuwa atalipeleka suala hilo kwenye vikao vya ngazi ya juu kwa maamuzi.
Kwa upande mwingine, Waziri Makamba amebaini kuwa Zanzibar kuna bandari zaidi ya 500 za majahazi, nyingi zikiwa ni bandari bubu zinazofanikisha magendo kutoka Zanzibar na Bara na Zanzibar na Kenya. Hali inayosababisha kukosekana kwa ukadiriaji halisi wa biashara kati ya Bara na Zanzibar.
Waziri Makamba amelitaka jukwaa la wakuu wa mikoa ya ukanda wa pwani (kwa Bara) na wakuu wa mikoa ya Zanzibar limalizie mchakato wa kuzifuta baadhi ya bandari hizo na kurasimisha chache ambazo zitakuwa na vituo vya forodha.
No comments:
Post a Comment