• YALIYOMO

    Thursday, 19 October 2017

    Sheikh Mkuu wa mkoa afariki



    Morogoro. Shinikizo la damu ambalo linaelezwa kuwa kwenye kundi la magonjwa yasiyoambukiza na kuongoza kwa kusababisha vifo kwa sasa, limemuua Sheikh wa Morogoro, Abdallah Mkang’ambe (48) ikiwa ni miezi 17 tangu achaguliwe kushika wadhifa huo.

    Akizungumzia kifo hicho, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, Rajabu Katimba alisema wamepoteza kiongozi tegemeo na kipenzi cha watu na kwamba, atazikwa leo Morogoro.

    Akitoa taarifa za kifo hicho jana, Kaimu Mwenyekiti wa Bakwata Morogoro, Sheikh Yahya Mrisho alisema Sheikh Mkang’ambe alianza kuugua wiki iliyopita na kulazwa katika hospitali ya rufaa Morogoro na baada ya hali yake kuwa mbaya alihamishiwa Hosptali ya Taifa Muhimbili (MNH).

    Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma MNH, Aminiel Elgeisha alieza kuwa hakuwa na taarifa za kifo hicho.

    Sheikh Mrisho alisema baada ya kifo hicho, Bakwata makao makuu kwa kushirikiana na ofisi ya mufti walikuwa wanafanya utaratibu wa kuusafirisha mwili kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kwamba, mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake maeneo ya Nanenane manispaa ya Morogoro.

    Sheikh Mkang’ambe alichaguliwa Mei mwaka jana.

    Watuma rambirambi

    Sheikh wa mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta alisema ameguswa na taarifa za kifo hicho hasa ikizingatiwa alikuwa kijana na tegemeo la Morogoro. “Tumempoteza kijana lakini ni mapenzi ya Mungu tuendelee kumuombea,” alisema.

    Naye Sheikh wa wilaya ya Morogoro, Abdalrahman Kiswabi alisema kifo hicho kimeacha pengo kwa waislam na Bwakata, kwani alikuwa ni kiungo na alipigania haki za waumini na kudumisha amani.

    Wengine walioguswa na kifo hicho ni Padri Luitfrid Mkseyo ambaye ni Katibu mkuu wa jimbo Katoliki Morogoro na katibu msaidizi wa kamati ya amani.

    Padri Makseyo alisema kanisa hilo na viongozi wa madhehebu mengine ya dini, limepata mshtuko kwa kuwa Sheikh Mkang’ambe alikuwa kiongozi aliyehubiri amani na upendo wakati wote bila ya kubagua dini. “Kwangu naweza kumzungumzia Sheikh Mkang’ambe kama dira yetu viongozi wenzake hata waumini,” alisema.

    Source: Mwananchi

    No comments:

    Post a Comment

    Contributors

    Powered By Blogger