Ujio wa Djuma ndani ya Simba unaongeza idadi ya makocha wa Burundi ndani ya ligi yetu na kufikia watatu. Nsanzurwimo Ramadhani (kocha mkuu Mbeya City), Etienne Ndayiragije (kocha mkuu Mbao FC) na Masud Djuma (kocha msaidizi Simba) hawa wote ni makocha wanaotoka taifa la Burundi.
Etienne Ndayiragije
Amefungua njia kwa makocha wa Burundi kuaminiwa katika kipindi hiki kutokana na mafaniko aliyoyapata akiwa na Mbao msiu uliopita, kwa mujibu wa mwenyekiti wa klabu hiyo Bw. Solly Njashi malengo ya klabu yao kwa msimu uliopita yalikuwa ni kubaki ligi kuu Tanzania bara na kufika hatua ya robo fainali ya Azam Sports Federation Cup.
Etienne alivuka malengo hayo baada ya kuifikisha Mbao fainali ya ASFC na kupoteza 2-1 kwa Simba May 2017 kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma, Mbao ilifanikiwa kusalia kwenye ligi licha ya kupambana hadi dakika za mwisho kukwepa mkasi wa kushuka daraja ambao mwisho wa siku uliwakumba wenzo wa jijini Mwanza Toto African pamoja na timu nyingine mbili ambazo ni JKT Ruvu na African Lyon.
Kocha wa Mbao amekuwa ni muumini wa vijana, tangu alipokuja Mbao hadi sasa bado msingi wa timu yake umejengwa na wachezaji vijana, msimu huu ana wachezaji wengi ambao wanacheza ligi kuu kwa mara ya kwanza aliowaunganisha na wazoefu wachache ambao pia hawana majina makubwa ndani ya nchi.
Mbao imekuwa ni timu ambayo inatoa ushindani mkubwa kwenye ligi wameifunga Yanga mara mbili msimu uliopita, mara ya kwanza ilikuwa ni mchezo wa nusu fainali ya ASFC kabla ya kuwachapa tena kwenye mechi ya mwisho msimu uliopita.
Nsanzurwimo Ramadhani
Ameanza kazi rasmi Mbeya City mwanzoni mwa mwezi huu baada ya kuondoka kwa Kinnah Phiri, bado hajaonesha cheche zake ameisimamia City kwenye kwa mara ya kwanza akiwa kocha mkuu ilipotoka sare ya kufungana 2-2 dhidi ya Mbao Ijumaa iliyopita uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Anabebwa na uzoefu wake katika soka la Afrika Mashariki pamoja na kusini mwa Afrika akiwa amefundisha vilabu vya mataifa mbalimbali Burundi, Rwanda, Botswana, Malawi, Uganda na Afrika Kusini. Amewahi kuwa mshauri wa benchi la ufundi kwenye timu ya taifa ya Burundi pia amewahi kuwa kocha wa muda wa timu ya taifa ya Malawi.
Masud Djuma
Alikuwa mchezaji katika vilabu tofauti vya Burundi na Rwanda lakini pia amewahi kucheza Seychelles kabla ya kuamua kuingia kwenye fani ya ukocha. Msimu uliopita (2016/2017) aliiwezesha Rayon Sport kushinda ubingwa wa ligi kuu ya Rwanda ‘Azam Rwanda Premier League’ ambapo pia alishinda tuzo ya kocha bora wa msimu huo.
Amejiunga na Simba kuwa kocha msaidizi chini ya Omog lakini tayari Burundi wameongeza idadi ya makocha kwenye ligi ya Tanzania. Burundi limekuwa taifa pekee lenye makocha wengi kwenye ligi ya Tanzania ukiachana na makocha wazawa. Makocha wengine wa kigeni ni Joseph Omog-Simba (Cameroon), George Lwandamina-Yanga (Zambia), Aristica Cioaba-Azam (Romania), Hans van Pluijm-Singida United (Netherland).
No comments:
Post a Comment